Mlinda Lango Chaguo la Kwanza wa Simba SC na Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Aishi Manula, amefanyiwa upasuaji Afrika Kusini alipoenda kwa ajili ya matibabu ya majeraha ya nyama za paja.
Manula aliondoka nchini Jumatatu (Mei 29) akiongozana na daktari wa klabu yake Edwin Kagabo kwa ajili ya kwenda kupata matibabu kutokana na jeraha lililomweka nje kwa muda mrefu.
Manula aliumia kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ walipocheza dhidi ya Ihefu kwenye Uwanja wa Azam Complex Aprili 7 mwaka huu, na tangu hapo alikuwa nje ya uwanja huku Mlinda Lango chaguo la tatu wa klabu hiyo, Ally Salim akicheza kwenye michezo iliyofuata.
Meneja wa machezaji huyo, Jemedari Said amesema, Manula alifanyiwa upasuaji juzi Jumanne (Mei 30) saa saba mchana kwa saa za Afrika Kusini ambayo ni sawa na saa nane mchana kwa saa za hapa nyumbani na kwa sasa anaendelea vizuri.
“Nimewasiliana naye muda mfupi baada ya kutoka chumba cha upasuaji yupo vizuri, kilichobaki sasa ni kupangiwa ratiba ya mazoezi pale daktari wake atakapoona inafaa,” amesema Jemedari.
Aidha, amesema kwa sasa hajui mchezaji huyo atakuwa nje ya uwanja kwa muda gani na wanasubiri maelekezo ya madaktari waliomfanyia upasuaji.
“Lini atarejea uwanjani nadhani hilo sasa ni jukumu la daktari wake aliyefuatana naye huko, atawasiliana na klabu yake kuwaeleza hali halisi jinsi ilivyo na wao ndiyo watakaotoa taarifa rasmi baadae ya lini atarejea uwanjani,” amesema Meneja huyo ambaye aliwahi kuzichezea timu za Kariakoo ya Lindi na 82 Rangers ya Shinyanga.
Hata hivyo habari za ndani zinasema Uongozi wa Simba SC umeanza mchakato wa kumsaka Mlinda Lango atakayeziba pengo la Manula hadi pale atakapokuwa fiti.
Mlinda Lango wa Vipers SC ya Uganda Alfred Mudekereza na Mlinda Lango wa Coastal Union Justin Ndikumana wanatajwa mmoja wapo kumrithi Manula.