Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando amethibitisha kutokea vifo vya watu 19, baada ya kutokea kwa ajali iliyohusisha gari aina ya Lori namba T 825 CMJ lililoigonga gari yenye nambari T 269 CJC aina ya Coaster.
Kamanda Kyando amesema kuwa ajali hiyo imetokea usiku wakuamkia leo majira ya saa 3 usiku katika eneo lenye mwinuko mkali katikati ya mpaka wa Mbeya na Mkoa wa Songwe ambapo mpaka sasa jeshi hilo linaendelea kuhakikisha barabara ya sehemu ajali ilipotokea inaweza kupitika.
“Ajali ilitokea mnamo majira ya saa 3.15 jana usiku baada ya gari aina ya lori kufeli breki na kuligonga kwa nyuma gari la aina ya Coaster lililokuwa na abiria 17 ambao wote walifariki hapohapo,”amesema Kamanda Kyando.
Amesema kuwa abiria wengine wawili akiwemo dereva wamefariki wakiwa hospitalini, lakini akatoa wito kwa madereva kufuata sheria za barabarani hasa wanapofika maeneo yenye mwinuko mkubwa, na amewaomba ndugu wajitokeze kuitambua miili ya ndugu zao.
Hata hivyo, kwa sasa miili ya watu hao 17 imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Mbozi kwa ajili ya uchunguzi.