Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Kalisti Lazaro amethibtitisha vifo vya watu watano na majeruhi tisa, vilivyokea kwa ajali ya gari Basi dogo aina ya Coaster iliyoacha njia na kupinduka katika Kijiji cha Mbaramo Tarafa ya Umba.

Amesema gari hilo lilikuwa likitokea Kijiji cha Mbaramo lilikokuwa limepeleka msiba kuelekea Mkoani Dar es salaam na kutaja majina ya waliofariki kuwa ni Sebastian Kamwedi (35), Msambaa Martin (70), Jackline Shemela (37), Emanuel Philipo na Elly Gumbo.

“Majeruhi sita wa ajali hii wamepelekwa Hospital ya Rufaa Bombo iliyopo Tanga na majeruhi watatu bado wanaendelea kupata matibabu katika Kituo cha Afya cha Mnazi kilichopo Lushoto,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Inadaiwa chanzo cha kutokea kwa ajali ya Basi hilo dogo Juni 10, 2022, ni baada ya dereva aliyekuwa akiliendesha kushindwa kumudu kupita kwenye kona kutokana na mwendo kasi, hali iliyopekea kupoteza mwelekeo na kupinduka.

Kufuatia ajali hiyo, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa madereva kuwa makini wanapopanda milima ya Usambara, kuzingatia sheria na alama za barabarani ili kuepusha kukatisha uhai wa watu, kuharibu mali na miundombinu.

Ajali hii inatokea ikiwa yamepita masaa kadhaa tangu kutokea kwa ajali nyingine Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa, baada ya Basi dogo la abiria aina ya Coaster kuligonga lori lililokua limeharibika na kusababisha vifo vya watu 20 na majeruhi wanane, Juni 10, 2022.

OACPS yatangaza neema kwa wakulima
Mtoto (10) ampiga risasi mwanamke aliezozana na mama yake