Jumla ya Watu wasiopungua 37 wamefariki baada ya kutokea kwa ajali ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika eneo la kijiji cha Jakana, kilichopo umbali wa kilomita 35 nje ya mji wa Maiduguri, kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Polisi wa usalama Barabarani katika jimbo la Borno wamesema ajali hiyo iliyohusisha mabasi mawili ilipelekea kutokea kwa mlipukona kusababisha moto mkubwa unaosadikika kusababisha watu wengi kuteketea.
Ajali hiyo, iliyotokea Kijiji cha Jakana, nje kidogo ya mji wa Maiduguri ambao ni makao makuu ya jimbo imetokea huku kukiwa na wasiwasi kuwa huenda idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na ukubwa wa tukio na majeruhi.
Polisi inasema sababu kuu ya kugongana kwa magari hayo ni mwendo kasi wa madereva na kupasuka kwa gurudumu la moja kati ya mabasi yaliyohusika ambapo muda mfupi kabla ya ajali hiyo vyombo vya habari viliripoti ajali nyingine katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja, iliyouwa watu 17.