Takriban watu 49 wamethibitishwa kufariki na wengine 50 wamejeruhiwa kufuatia ajali mbaya ya barabarani, iliyotokea katika eneo la makutano ya barabara ya Londiani kando ya barabara kuu ya Nakuru – Kericho nchini Kenya.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Mkuu wa Mkoa wa Bonde la Ufa, Abdi Hassan alisema idadi ya waliofariki inaweza kuongezeka, na kwamba ilihusisha lori lililokuwa likitoka Nakuru kuelekea Kericho ambalo lilipoteza mwelekeo na kugonga mabasi madogo ya abiria (matatu), magari binafsi na pikipiki kabla ya kuanguka kwenye mtaro.
Lori hilo, pia liliwagonga wachuuzi waliokuwa wakiuza mahindi ya kuchoma, Wafanyabiashara wa mbogamboga, kabichi na machungwa kando ya barabara kwenye njia ya kuelekea Muhoroni na kudai kuwa baadhi ya miili ilikuwa imenasa katika vyuma vya magari.
Mkuu wa Polisi wa Londiani, Agnes Kunga alisema mara baada ya tukio ni watu 20 walifariki papo hapo na wengine waliendelea kufariki wakati wakipatiwa matibabu katika vituo mbalimbali vya afya vya Nakuru na Kericho.
Alisema, “tumepoteza zaidi ya watu 20 wengine wamekimbizwa hospitali kaunti ndogo ya Molo na hospitali za Nakuru Level Five, ni ajali mbaya sana. Watu kadhaa wanahofiwa kufariki huku wengine wakiwa wamenasa kwenye mabaki kwenye mrundikano huo.”
Tayari Viongozi wa Kenya akiwemo Rais William Ruto, wametoa salaam za rambirambi kwenye mitandao ya kijamii, huku watu wengi wakiweka picha za mshumaa huku takwimu za Mamlaka ya Kitaifa ya Uchukuzi na Usalama nchini Kenya, ikisema takriban watu 21,760 walihusika katika ajali za barabarani mwaka 2022, na 4,690 walifariki.