Ajali iliyotokea hii leo Novemba 13, 2022 ikihusisha Basi la Arusha express ya kugongana na Lori la ujenzi eneo la Veyula – Makutupora, nje kidogo ya jiji la Dodoma imesababisha vifo vya Watu watano na wengine kadhaa kujeruhiwa.
Akithibitisha kutokea kwa ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Martin Otieno amesema bado wanafuatilia chanzo cha ajali na athari zaidi zilizotokana na tukio hilo.
Amesema, “Ni kweli ajali hiyo ipo, watu watano wamepoteza maisha katika eneo la ajali na wengine kujeruhiwa na wamekinbizwa hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa matibabu.”
Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda wamesema ajali hiyo ilisababishwa na mwendokasi na kwamba kuna vifo na majeruhi huku wakionya madereva kuwa makini hasa wanakuwa wamepakia abiria.