Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, DCP Lucas Mkondya amethibitisha vifo vya watu watano vilivyotokea kijiji cha chigweje Wilaya ya Nanyumbu, kufuatia ajali ya gari iliyopinduka na kuwaka moto na kusababisha watu hao kuungua mpaka kufa ambapo mmoja ni dereva wa gari wengine wanne hawajatambulika hivyo amewaomba wananchi kujitokeza ili kuwatambua ndugu zao.
”Tunaomba wananchi wanaohisi kupotelewa na ndugu zao ambao walikuwa wanatambua kwamba jana walikuwa na safari ya kutoka ya mangaka kwenda Tunduru na kama hawajafika nyumbani basi waende Hospitali ya Mkoa ya wilaya Masasi kwa ajili ya kutazama miili hiyo” Mkondya.
Vifo hivyo ni kufuatia ajali ya gari iliyotokea jana majira ya saa 10 jioni ikihusisha gari aina ya Toyota Noah yenye namba za usajili T.485 DJE iliyokuwa inafanya safari zake kutoka Mangaka kwenda Tunduru ambapo gari hiyo iliacha barabara na kuanguka kisha kuwaka moto eneo la Lumsule ambalo lina kona na mteremko mkali katika barabara ya Mangaka Tunduru kijiji cha chigweje Wilaya ya Nanyumbu Mkoani Mtwara.
Aidha kondakta wa gari hiyo Khalid aliruka kutoka kwenye gari hiyo kabl aya kutokea kwa ajali na sasa anashikiliwav na polisi kwa lengo la kusaidia kukamilisha upelelezi.