Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Khamis Hamza Chilo amewahasa Madereva wa Bodaboda Visiwani Zanzibar kufuata Sheria Za Usalama barabarani ili kuepusha ajali na vifo vilivyoshamiri.

Rai hiyo imetolewa leo Agosti 10, 2021 na Naibu Waziri Chilo wakati wa kikao na madereva bodaboda wa Mkoa wa Mjini Magaharibi ambacho pia kilihudhuriwa na uongozi wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi.

“Serikali yenu Sikivu chini ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi iko katika mchakato  ili mruhusiwe kutoa huduma za usafiri katika maeneo mbalimbali ya Zanzibar sasa nawaomba muanze kujifunza na kufuata sheria za usalama barabarani ili tunayoona yanayotokea kule Bara yasitokee huku.” Amesema Naibu Waziri Chilo.

Akizungumzia takwimu za ajali za bodaboda, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Kamishna Msaidizi wa Polisi Awadh Juma Haji amesema vifo vitokanavyo na ajali za bodaboda vimepungua kutokana na elimu inayotolewa kwa madereva hao.

“Mwaka huu tuna ajali 17, watu waliofariki mwaka jana ni watu 18 na mwaka huu tuna vifo 17 huku upungufu ukiwa ni mtu mmoja, lakini ajali zilizosababisha majeruhi kwa mwaka jana ni ajali 19 na mwaka huu ni ajali 6 kwa hiyo kuna upungufu wa ajali 15, watu waliojeruhiwa mwaka jana watu  37 na  mwaka huu  ni watu 6 kwahiyo tunaona kuna kushuka kwa ajali na athari zake,” Amesema RPC Awadh.

Nao madereva bodaboda wameiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa nia ya kuandaa utaratibu ili waweze kuruhusiwa kufanya kazi zao Visiwani hapo huku wakiahidi kuendelea kufuata sheria za usalama barabarani.

Tanzania nchi ya 22 kusaini mkataba wa uanzishwaji taasisi uthibiti wa dawa AU
Mabula asikitishwa wamiliki kutolipa gharama za upimajitoa