Wakala wa ufundi na umeme nchini (TEMESA), unakusudia kuendelea kutoa elimu kwa wasimamizi na watumiaji wa vivuko maeneo mbalimbali kabla ya kuanza kwa safari itakayojumuisha matumizi ya vifaa vya kujiokoa endapo kutatokea dharura au ajali.
Hayo yamebainishwa leo, Novemba 14, 2019 jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (TEMESA), Mhandisi Japhet Masele alipokuwa akizungumzia mafanikio ya sekta hiyo chini ya Serikali ya Awamu ya Tano ikiwemo dira, dhima na majukumu yake.
Amesema mafunzo hayo pia yatalenga matengenezo kwa vivuko mara kwa mara, kutoa kinga kwa watumishi, kufunga vifaa mbalimbali kwa ajili ya kuboresha usalama katika maeneo ya vivuko, ufungaji wa kamera, kuongeza vifaa vya kujiokolea na kuandaa mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa mienendo ya vivuko.
“Hali hii itasaidia wafanyakazi na watumiaji wa vivuko kuoata uelewa juu ya nini.cha kufanya wanapokabiliwa na dharula yeyote lakini pia mfumo huu utadhibiti uzito wa abiria na mizigo iliyobebwa kwenye vivuko maana haya ni mambo ya msingi katika kupunguza hatari na ajali,” amefafanua Injinia Masele.
Akizungumzia mafanikio yao kwa miaka minne chini ya awamu ya tano ya Rais John Magufuli, Mhadisi Masele amesema wameendelea kuboresha na kusimamia uendeshaji wa vivuko vya serikali na kuongeza idadi toka vivuko 13 kati ya mwaka 2005 hadi 30 kwa vituo 19 nchini ongezeko ambalo ni sawa na asilimia 131.
Ameongeza kuwa wakala umefanikiwa kununua vivuko vitatu ambavyo ni MV Kazi cha jijini Dar es salaam kilichonunuliwa kwa shilingi bilioni 7.3, MV Mwanza shilingi bilioni 8.9 na MV Tanga shilingi bilioni 4.02; na kufanya jumla ya gharama zote kuwa ni shilingi bilioni 20.22.
“Pia tumenunua boti tano nchini ikiwemo kile cha Mkoani Mtwara MV Kuchele, Mkoa wa Pwani MV Mkongo, Mkoa wa Tanga kuna MV Bweni na Mv Sar III ambavyo vyote kwa pamoja vimegharimu kiasi cha shilingi milioni 415,” amefafanua Injinia Masele.
Kuhusu uboreshaji wa karakana, Masele amesema hadi sasa Wakala una idadi ya karamana 26 katika mikoa yote nchini na kwamba tayari katika wilaya wamekamilisha karakana moja iliyopo wilaya ya Kilombero ili kusogeza huduma kwa wateja wa wilaya za mrimba, Malinyi na Ifakara.
Aidha, amesema wameanzisha karakana inayotembea ikiwa imegharimu kiasi cha shilingi milioni 95 itakayohudumu Mkoani Dar es salaam. Itahudumu kwa magari ya Bohari ya Dawa (MSD) yapatayo 100, Mkoa wa Pwani katika wilaya za Bagamoyo, Utete, Mkuranga na Kisarawe.
TEMESA) ilianzishwa chini ya Sheria ya Wakala Na. 30 ya Mwaka 1997 na kuzinduliwa rasmi na Serikali Juni 23, 2006 kwa malengo ya kutoa huduma bora na kwa ufanisi katika nyanja za uhandisi mitambo, umeme, elektroniki na uendeshaji wa vivuko.