Kiungo mpya wa Azam FC Ibrahim Ajibu amesema hana budi kucheza kwa kujituma zaidi kila anapopata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza, ili kulishawishi Benchi la Ufundi kuingia kwenye mfumo wa kiufundi.
Ibrahim Ajibu alijiunga na Azam FC juma lililopita, baada ya kufikia makubaliano na Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC ya kuvunja makataba wake, kufuatia kukosa nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha klabu hiyo.
Baada ya kucheza mchezo wake wa kwanza akiwa na Azam FC kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi dhidi ya Meli 4 City iliyokubali kufungwa bao 1-0, Ajibu amesema amefurahishwa na hatua hiyo, lakini anaamini kuna kazi kubwa iliyo mbele yake ili kutimiza lengo la kuingia kwenye mfumo na acheze kwenye kikosi cha kwanza.
“Kuna vijana wengi kwenye timu nimewakuta na wana uwezo mkubwa wa kucheza mpira, kwa hiyo na mimi ni lazima nipambane ili niingie katika kikosi moja kwa moja, hii inanipa changamoto kidogo, lakini siyo sana, kwa sababu sasa hivi nimekomaa, kipindi kile nilikuwa bado mdogo,” amesema Ajibu.
Kiungo huyo ambaye ni zao la kikosi cha pili cha Simba (Simba B), aliwahi kupelekwa kwa mkopo Mwadui FC ya Shinyanga lakini alirejeshwa mwaka 2017 huku ilipofika 2019, akatimkia kwa wapinzani wao, Young Africans.
Alikaa kwenye klabu hiyo kwa msimu mmoja, akarejea nyumbani Simba SC, mpaka Desemba 30, mwaka jana alipojiunga rasmi na Azam FC, akichukua nafasi ya Abubakar Salum ‘Sure Boy’ aliyetimkia Young Africans.