Majonzi yametawala mitandaoni hususan kwa raia wa Kenya baada ya msichana mwenye umri wa miaka 28 kujinyonga hadi kufa muda mfupi baada ya kuandika ujumbe kwenye Facebook.
Millicent Kithinji Mwiriki, mkaazi wa kijiji cha Gaturi amesababisha mshtuko na taharuki baada ya baba yake kumkuta akiwa ananing’inia kwenye kamba akiwa ameshakata roho, Alhamisi iliyopita, saa chache tangu aandike kwenye ukurasa wake wa Facebook jumbe za kumuaga mwanaye mwenye umri wa miaka mitatu pamoja na baba yake.
Ujumbe wa kumuaga mwanaye unasomeka, “mwanangu mpendwa, siwezi kuwa na maneno ya kueleza jinsi ninavyokupenda. Nimepambana vita, lakini inaonekana kama ninakaribia kushindwa. Ninakuombea Mungu akupe ulinzi, malezi, upendo na faraja. Mama bado anakupenda, na siku zote atakupenda, tafadhali nisamehe.”
Ujumbe huu pia ulitanguliwa na ujumbe aliouandika saa tisa mchana kwa ajili ya baba yake, “Baba, samahani, lakini siwezi kutoa hii habari kuwa ninajiandaa kujiua. Natumaini moyo wako utanisamehe.”
Msichana huyo msomi, mhitimu wa stashahada ya ugavi na ununuzi kutoka Chuo Kikuu cha Jomo Kenyata cha Kilimo na Sayansi (JKUAT), anadaiwa kufikia uamuzi huo baada ya kupokea ujumbe wa simu kutoka kwa mwanamke mmoja mwenye uhusiano wa kimapenzi na mzazi mwenzake.
Familia yake imeiambia Citizen kuwa ujumbe huo ndio uliompasua moyo kwani alikuwa akiishi kwa matumaini akimsubiri mzazi mwenzie amalize chuo ili atimize ahadi ya kumuoa.
“Nina mimba ya mumeo, ni muda muafaka sasa wa kukubaliana na hali na kuendelea na maisha yako, na hakuna uwezekano wa yeye kurudiana tena na wewe,” Citizen wamenukuu sehemu ya ujumbe huo mfupi wa simu ulioandikwa kwa lugha ya kiingereza.
Aidha, baba yake alieleza kuwa hali ya ugumu wa maisha na kukosa ajira pia vilichochea kufikia uamuzi huo.
Jeshi la polisi limethibitisha kutokea tukio hilo la kujiua kwa msichana huyo na kueleza kuwa linaendelea kufanya upelelezi.