Utafiti mpya ulifanywa na shirika la kazi la Umoja wa Mataifa ILO umeonesha wanawake wamekuwa waathirika wakubwa kwenye ajira na kukosa kipato sababu maeneo wanayofanyia kazi ndio yameathirika zaidi na janga la Corona mfano kwenye sekta ya malazi, chakula na utengenezaji.
Utafiti umeonesha kati ya mwaka 2019 na 2020 ajira kwa wanawake zimepungua kwa asilimia 4.2 duniani, ikiwakilisha ajira milioni 54, wakati wanaume wameathirika kwa asilimia 3 ikiwakilishwa na ajira milioni 60.
Kupitia utafiti huo inaonyesha kutakuwa na upungufu wa wanawake milioni 13 katika ajira mwaka huu ikilinganishwa na mwaka 2019, ilihali idadi wa wanaume katika ajira inatarajiwa kuongezeka kwa viwango vilivyo onekana katika miaka miwili.
Hali kadhalika asilimia 43 tu ya wanawake walio kwenye umri wa kuajiriwa ndio watakaopata ajira mwaka 2021, ikilinganishwa na asilimia 69 ya wanaume ambao wanatarajiwa kupata ajira mwaka huu.
Sambamba na hayo Sio kila bara limeshuhudia hali mbaya kwakufanana, kwa mfano, utafiti umeonesha ajira huko bara la Amerika zimeathirika vibaya, kiwango cha ajira kimeshuka kwa zaidi ya asilimia 9,inafuatiwa na nchi za kiarabu ambazo ajira zimeshuka kwa zaidi ya asilimia 9, ikifuatiwa na bara la Asia Pasifiki kwa asilimia 3.8.
Huku Bara la ulaya limeshuhudia anguko la ajira kwa asilimia 2.5, Asia ya kati ikiwa na asilimia 1.9 ya kiwango cha ajira zilizopotea na kwa upande wa Afrika, ajira kwa wanaume zimepungua kwa asilimia 0.1 kati ya mwaka 2019 na 2020, wakati ajira za wanawake zikipungua kwa asilimia 1.9.