Asasa mbalimbali za kiraia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaotetea haki za watoto wametoa wito kwa serikali kwa kushirikiana na mahakama kusimamia haki za watoto na kuhakikisha ajira kwa watoto zinakoma.
Wito huo umetolewa leo Juni 12, 2021 katika maadhimisho ya siku ya kutokomeza ajira kwa watoto, yaliyofanyika kituo cha watoto wetu kilichopo Mbezi, Mkoani Dar es Salaam ambacho kinajihusisha na malezi ya watoto wanaishi katika mazingira hatarishi.
Wiki iliyopita, Umoja wa Mataifa ulitoa ripoti iliyoeleza kuwa ulimwengu kwa mara ya kwanza umeshuhudia ongezeko la idadi ya watoto wanaofanyishwa kazi katika kipindi cha miongo miwili.
Katika ripoti ya pamoja, Shirika la Kazi la Kimataifa, ILO na lile la Umoja wa Mataifa UNICEF, idadi hiyo ya watoto wanaotumikishwa ilifikia milioni 160 mwanzoni mwa mwa mwaka 2020, ikiwa ni ongezeko la watoto milioni 8.4 katika miaka minne.
Kuongezeka huko kulianza kabla ya kuzuka janga la corona na kunaonyesha mabadiliko makubwa ya muenendo ambao ulikuwa umeshuhudia idadi ya ajira kwa watoto ikipungua kwa milioni 94 kati ya mwaka wa 2000 na 2016.
Ripoti hiyo imesema wakati mgogoro wa COVID-19 ulianza kushika kasi, karibu mmoja kati ya watoto 10 ulimwenguni alifanyishwa kazi, huku eneo la kusini mwa jangwa la Sahara likiathirika pakubwa kutokana na ongezeko la idadi ya watu, migogoro na umaskini.