Ajuza mwenye umri wa miaka 107, raia wa Iran aliyekuwa ameambukizwa virusi vipya vya corona (covid-19) amepona, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari vya nchini humo.
Mwanamke huyo alitajwa kwa jina la Saltanat Akbari alikuwa amelazwa katika hospitali ya Khansari iliyo katika jiji la Arak. Bibi Akbari Ameruhusiwa kutoka hospitalini baada ya kukaa kwa muda akiwa ametengwa kwa utaratibu maalum huku akipatiwa matibabu.
“Ameshinda virusi vya corona baada ya kupewa msaada wa karibu na madaktari pamoja na wauguzi wengine hospitalini,” gazeti la Fars limeeleza.
Iran ni moja kati ya nchi zilizoathirika zaidi na maambukizi ya covid-19 katika ukanda wa Mashariki ya Kati, ikiwa na jumla ya visa 133,521 vilivyothibitishwa na vifo 7,359 vilivyotokana na virusi hivyo.
Kwa mujibu wa wataaalam ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO), virusi hivyo huwaathiri zaidi wazee na watu wenye magonjwa mengine ambao kinga zao zimeathiriwa na sababu mbalimbali.