Mtandao wa Facebook jana ulidukuliwa na watu wasiojulikana, ambapo akaunti za watu milioni 50 ikiwa ni pamoja na ya mmiliki wa mtandao huo, Mark Zuckerberg ziliingia mikononi mwa wadukuzi.
Tukio hilo ni baya zaidi dhidi ya usalama wa watumiaji wa mtandao huo kuwahi kutokea likiwapa wadukuzi nafasi ya kuziingilia akaunti za watu wengi zaidi pamoja na viongozi wa mtandao huo.
Facebook ambayo ina watumiaji zaidi ya bilioni 2.2 kwa mwezi imesema kuwa bado haijabaini ni kwa kiasi gani wadukuzi walitumia vibaya akaunti hizo pamoja na taarifa binafsi za watumiaji.
Mtandao huo pia umeleza kuwa bado haujabaini eneo walipo wadukuaji hao na kama kuna watu maalum ambao walikuwa wanawalenga.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mark Zuckerberg amesema kuwa tukio hilo lilikuwa baya zaidi hata kwake, kwani mbali na akaunti yake akaunti nyingine iliyodukuliwa ni ya Afisa Mkuu wa Oparesheni wa Mtandao huo, Sheryl Sandberg.