Mamlaka ya kijeshi ya Guinea, imeamuru benki kufungia akaunti zote zinazohusiana na serikali ili kupata mali za serikali.
Hatua hiyo imejiri baada ya viongozi wa jeshi kusema wanataka kumaliza ufisadi uliokithiri, ukiukwaji wa haki za binadamu na usimamizi mbaya, baada ya kuchukua udhibiti wa Serikali ya Rais Alpha Conde mwishoni mwa wiki iliyopita.
Jeshi limesema agizo hilo linaathiri akaunti za taasisi na watu binafsi kwa serikali inayomaliza muda wake, wakiwemo maofisa wa serikali ya Rais aliyeondolewa madarakani Alpha Condé.
Jumuiya ya kiuchumi ya eneo la Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) ambayo inataka katiba kufuatwa imetuma ujumbe wa kufanya mazungumzo na mamlaka ya Guinea na kutaka Conde aachiwe huru.