Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani linamshikilia, Shabani Athumani (61) mkazi wa Kwamakocho, Chalinze akituhumiwa kumiliki kiwanda cha kutengenezea silaha mbalimbali za moto.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Wankyo Nyigesa, amewaambia waandishi wa habari kuwa tukio la kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo limetokea Januari 31, saa 1 jioni.
Kwa mujibu wa Nyigesa, mtuhumiwa huyo alikamatwa kutokana na ushirikiano wa raia mwema na kwamba baada ya kupata taarifa hizo walifanya uchunguzi na kisha kubaini uwepo wa kiwanda hicho.
Amesema katika uchunguzi huo Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa huyo akiwa na mtambo wa kufulia vyuma, chupa 5 ndogo zenye baruti ndani yake, Fataki 48 na risasi 42 za bunduki aina ya Gobole na Paketi 1 ya unga wa Kiberiti.
Nyigesa ametaja vifaa vingine kuwa ni mitambo mitatu ya Silaha aina ya gobole ambayo ipo tayari bado kuwekwa mtutu na kitako, mitambo ya kutobolea vifaa vya miti vinavyotumika kwenye silaha aina gobole na kopo moja lenye unga wa tindikali ambalo unatumika kuunganisha vyuma vinavyofungwa kwenye silaha aina ya gobole.