Mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu mkazi wa kijiji cha Keringet kaunti ya Pokot nchini Kenya amekutwa na sindano 7 za kushonea kwa mkono tumboni mwake, baada ya kupigwa picha ya xray
Mtoto huyo alipelekwa hospitali ya Kapenguria siku ya Jumanne kupata matibabu ya maumivu ya tumbo ambayo alikuwa akiyapata kwa muda mrefu bila kujua tatizo ni nini.
Aidha, Bibi wa mtoto huyo, Emily Linga’a ambaye ndiye anayeishi naye, amesema mtoto huyo alikuwa akilalamika maumivu ya tumbo kwa zaidi ya miaka miwili, lakini hawakuweza kubaini mara moja chanzo cha maumivu hayo na kuendelea kumpatia dawa za kutuliza maumivu, lakini baada ya kuona anazidi kulalamika walimpeleka hospitali na kugundua ana tatizo hilo.
“Kwanza nilidhani mtoto alikuwa na minyoo, sikuwahi kufikiria kwamba ana sindano tumboni mwake, nilikuwa nahisi ni malaria siku zote na kumpa dawa za maumivu”, amesema bibi huyo ambaye anaishi naye, baada ya mama yake kumuacha alipoolewa na mwanaume mwengine.
Hata hivyo, Madaktari wa hospitali hiyo wamempa rufaa ya kwenda hospitali kubwa ya Moi ili kuweza kufanyiwa upasuaji wa tumbo, na kutolewa sindano hizo ambazo hazijajulikana zimeingiaje.