Familia ya mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwiline aliyeuawa kwa risasi na askari polisi imetoa ratiba ya mazishi yake.
Akizungumza jana baada ya kupokea ripoti ya mwili wa marehemu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, kaka wa marehemu, Moi Kiyeyeu alisema kuwa mdogo wake ataagwa Alhamisi wiki hii katika viwanja vya NIT eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam.
Alisema baada ya kuagwa katika eneo hilo, siku hiyo-hiyo atasafirishwa kwenda Rombo-Mashati mkoa wa Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi.
Kwa mujibu wa ndugu, ripoti ya uchunguzi waliyopewa na madaktari wa Muhimbili inaonesha kuwa marehemu alipigwa risasi kichwani iliyoingia upande wa kushoto kutokea upande wa kulia.
“Ripoti tuliyopewa inaonesha kwamba kichwa cha marehemu kilipasuliwa na risasi ambayo iliingia upande wa kushoto na kutokea upande wa kulia ambao umefumuliwa vibaya,” shemeji wa Akwilina, Festo Kavishe anakaririwa na Mwananchi.
- Wanafunzi wa kike wawatoroka Boko Haram shuleni
- Trump ataka sheria ya umiliki wa silaha ifanyiwe marekebisho
Jeshi la polisi linawashikilia askari wake sita kwa uchunguzi kutokana na tukio hilo lililotokea Februari 16, Kinondoni jijini Dar es Salaam.