Uongozi wa Simba SC ni kama umewashtukia wapinzani wao kwenye mashindano ya Africa Football League (AFL), Al Ahly ambao wamewazuia nyota wao kwenda kwenye majukumu ya timu zao za taifa na sasa wekundu hao wameamua kuingia kambini leo Alhamis (Oktoba 12) kujiandaa na mchezo huo.
Wachezaji wa Simba SC awali walipewa mapumziko mafupi baada ya Ligi Kuu kusimama kupisha michezo ya kimataifa ya kalenda ya FIFA.
Uongozi wa Simba SC sasa umepanga kuwasiliana na mashirikisho ya soka katika nchi ambazo wachezaji wake wameitwa kwa ajili ya majukumu ya timu za taifa, kuyaomba kuwaruhusu kurejea nchini mapema kujiunga na kambi ya timu hiyo.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally, amesema kuwa wameamua kuchukua maamuzi hayo kutokana na umuhimu wa mchezo huo wa ufunguzi wa mashindano hayo utakaochezwa Oktoba 12 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
“Huu mchezo ni mkubwa, wenzetu wameamua kuwazuia wachezaji wao kwenda kujiunga na timu zao za taifa, na sisi kwa kuuchukulia kwa uzito mkubwa mchezo huu, tumeanza mchakato wa kuwasiliana na mashirikisho ya soka ambayo wachezaji wetu wameitwa kujiunga na timu zao za taifa, tutawaomba wawaachie warejee na kwa wale ambao hawajaenda wasiende ili waingia kambini kujiandaa na mchezo huu,” amesema Ahmed na kuongeza,
“Hii mechi yetu itakuwa ngumu kwa sababu ya ubora wa kikosi cha wapinzani wetu, Al Ahly wanaifahamu Simba SC kwa sababu wamewazuia wachezaji wao kwenda kwenye majukumu ya mataifa yao kwa ajili yetu na sisi tumeshtukia hili, kumfunga Al Ahly si jambo geni bali tunahitaji kumtoa mpinzani wetu katika mashindano haya kwa kusaka ushindi hapa nyumbani na Ugenini,” amesema Ahmed na kusisitiza Wanasimba kuungana ili kufanikiwa lengo lao la kusonga mbele katika michuano hiyo.
Ameongeza kuwa maandalizi ya ndani na nje ya uwanja kuelekea kwenye mchezo huo mkubwa Afrika yanaendelea vizuri na wanapata ushirikiano mzuri kutoka kwa Serikali na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).
“Hapo awali michuano hii ilijulikana kama Super League lakini sasa wanaiita Afrika Football League ambayo ni michuano mikubwa Barani Afrika na inashirikisha watu bora pekee ambao Simba SC ndio ni timu pekee katika ukanda huu wa soka wa Afrika Mashariki na Kati, haya mashindano hayako kwa bahati mbaya, bali Simba SC imepambana na kuvuja jasho hadi imefika kushiriki michuano hii mikubwa.