Pamoja na Klabu ya Manchester United kuonekana ipo kwenye hatua nzuri kuipata huduma ya kiungo wa Fiorentina, Sofyan Amrabat, taarifa zinadai dili hilo huenda likapinduka muda wowote kuanzia sasa baada ya matajiri wa Al-Hilal kuanza mazungumzo na wawakilishi ili wamsajili katika dirisha hili.
Taarifa zinaeleza kwamba dili hilo linaweza kugeuka kwa sababu Al-Hilal wamepanga kumuwekea mshahara mnono zaidi fundi huyu mwenye umri wa miaka 26, na kumalizana na Fiorentina mapema kwenye masuala ya ada ya uhamisho.
Man United ambayo ndio ilikuwa ya kwanza kwenye harakati za kuiwania huduma ya fundi huyu imekuwa ikisuasua kwenye masuala ya ada ya uhamisho kutokana na bajeti yao katika dirisha hili kuwa ndogo.
Hata hivyo, Mashetani Wekundu wana jeuri kwamba watampata Amrabat kwa sababu mchezaji huyo ameonyesha kupendezwa na mipango yao na amekuwa kwenye mawasiliano ya karibu na kocha wao Erik Ten Hag.
Staa huyu ambaye ni miongoni mwa wachezaji tegemeo katika kikosi cha kwanza cha Fiorentina amekuwa akihitajika na timu nyingi Barani Ulaya, baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye Fainali za Kombe la Dunia mwaka jana, akiwa na timu ya taifa ya Morocco kule nchini Qatar.