Wapinzani wa Young Africans katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Al Hilal ya Sudan, wameanza safari ya kuelekea Dar es salaam-Tanzania wakipitia DR Congo.
Miamba hiyo ya Afrika Mashariki na Kati itakutana katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika Jumamosi (Oktoba 08), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha itamalizia mjini Khartom-Sudan kwenye mchezo wa Mkondo wa Pili kati ya Oktoba 14-16.
Al Hilal inayonolewa na Kocha mwenye uzoefu wa Soka la Afrika Florent Ibenge, imeelekea DR Congo ambako itaweka Kambi kwa siku kadhaa kabla ya kuendelea na safari ya Dar es salaam- Tanzania.
Ikiwa DR Congo, Al Hilal itacheza michezo miwili ya Kimataifa ya Kirafiki dhidi ya TP Mazembe na AS Vita, ambazo pia zinajiandaa na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Al Hilal ilisonga mbele katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa faida ya bao la ugenini dhidi ya Mabingwa wa Soka wa Ethiopia St George, ikitanguliwa kufungwa 2-1 ugenini na kushinda nyumbani Khartoum-Sudan 1-0.
Young Africans ambayo ndio Bingwa wa Tanzania Bara, ilisonga mbele kwenye Michuano hiyo kwa kuibamiza Zalan FC kutoka Sudan Kusini kwa matokeo ya jumla 9-0. Ikishinda 4-0 kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza, kisha ikashinda 5-0 katika mchezo wa Mkondo wa Pili.