Kundi la kigaidi la Al-shabaab la nchini Somalia limeripotiwa kuendesha mafunzo kwa wazee na kufanya mashindano ya kulenga shabaha kwa kutumia bunduki.
Tovuti yenye uhusiano na kundi hilo imeweka picha za wazee wenye umri kati ya miaka 60 na 80 wakionekana wamebeba bunduki aina ya AKA 47 wakiwa wanalenga shabaha wakizungukwa na umati wa watu wanaoshuhudia.
“Kila mzee alipewa risasi tatu na alitakiwa kulenga shabaha iliyokuwa hatua 60 mbele,” mwandishi wa redio iitwayo Andalus amesema. “Kila mzee alihudhuria mafunzo ya awali kabla ya kushiriki mashindano,” aliongeza.
Tovuti hiyo imeweka picha zinazowaonesha wazee hao wakiwa wanaelekezwa na wanaume waliojificha sura zao. Katika picha nyingine, wazee hao wanaonekana wakiwa wamelala chini wakijaribu kulenga shahaba.
Imeelezwa kuwa lengo la hatua hiyo ya Al-Shabaab ni kutaka kuwashawishi wanavijiji wa eneo hilo kuwaunga mkono katika itikadi zao za kigaidi dhidi ya Serikali.