Kundi la Kigaidi la al-Shabab limekiri kuhusika na mauaji makubwa katika shambulizi la kambi ya walinda amani wa Umoja wa Afrika nchini Somalia na kumewaua wanajeshi wapatao 170 wa AU, wengi wao wakiwa wametokea nchini Burundi pia kuwaweka mateka wengine bila kutaja idadi yao.
Pamoja na taarifa hizo hata hivyo pande zote mbili zimekuwa zikitoa taarifa zinazokidhana juu ya idadi za vifo ikiwa jeshi la Burundi limesema kuwa wanajeshi wake 10 ndio waliopoteza maisha na wengine watano waliopotea.
Mashambulizi hayo katika eneo la Shabelle ya Kati nchini humo yalishuhudia wapiganaji waliokuwa na silaha nzito wakivamia kambi ya al-Baraf kilomita 160 kaskazini-mashariki mwa mji mkuu, Mogadishu, ambako vikosi vya Burundi, vinavyohudumu chini ya AU, viliweka kambi.
Wananchi wa eneo hilo wanadai kusikia milio ya silaha nzito asubuhi.
“Shambulizi limetokea jana asubuhi,,” Mjumbe wa AU, ambaye hakutaka kutambulika akiiambia BBC. “Magari mawili yaliyokuwa na mabomu na silaha yaliingia kwenye eneo na hapo ndio milio ya risasi ikaanza kusikika. Sifahamu idadi kamili ya waliopoteza maisha kwenye shambulizi lilitokea.”
Mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat amesikitishwa na shambulizi hilo pia ametoa pole zake kwa askari waliofariki na kusema kuwa “Waliopoteza maisha hawatasahaulika kamwe”.
Serikali ya Somali nayo imelaani vikali shamblizi hilo lililotokea na imeitaka Atmis wakishirikiana na jeshi la Somalia kujilinda dhidi ya wanamgambo wa al-Shabab.
“Tunatanguliza pole zetu kwa wahanga wa shambulizi la kigaidi, wa familia za marehemu, kwa Umoja wa Afrika na kwa washirika, Serikali na watu wa Burundi,” Taarifa ya serikali ya Somalia.
Pia imetoa wito kwa mashirika ya kimataifa na nchi za magharibi kutoa msaada zaidi wa kupambana na ugaidi.
Hili linatajwa kuwa ndio shambulio kubwa zaidi katika miaka ya hivi karibuni, pia ni shambulio la kwanza kwa Atmis tangu kuchukua nafasi ya jeshi la zamani, linalojulikana kama Amisom.
Kikosi hicho kimsingi ni sawa na jina jipya lakini chini ya azimio la Umoja wa Mataifa, Atmis inapanga kupunguza polepole viwango vya wafanyikazi kutoka 20,000 hadi sifuri ifikapo 2024.