Tume ya uchaguzi ya Ivory Coast imemtangaza Alassane Outtara kama mshindi wa kiti cha Urais, kwa kupata ushindi wa kishindo wa asilimia 94.27 ya kura zilizopigwa katika uchaguzi wa rais uliofanyika nchini humo siku ya Jumamosi .

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa na Rais wa tume hiyo huru ya uchaguzi Ibrahime Coulibaly-Kuibert leo Jumanne watu waliojitokeza kupiga kura walikuwa ni asilimia 53.90 na Alassane Ouattara amepata kura milioni 3,031,483 kati  ya kura zote zilizopigwa ambazo ni sawa na asilimia 94.27.

Taifa hilo kwa sasa lina kipindi kifupi cha kusubiri kama kuna changamoto au malalamiko yoyote yatakayojitokeza wakati matokeo hayo ya uchaguzi yanasubiri kuhalalishwa na baraza la katiba ya nchi hiyo.

Ouattara mwenye umri wa miaka 78 amepata zaidi ya asilimia 90 ya kura katika mikoa mingi ya nchi hiyo, ingawa vyama vya upinzani vinasema kwamba mpango wake wa kubakia madarakani upo kinyume na sheria.

Katiba ya Ivory Coast inaweka ukomo wa kipindi cha Urais kwa mihula miwili, lakini Ouattara anasema marekebisho ya katiba ya mwaka 2016, yanamruhusu yeye kuanza upya mamlaka yake ya Urais.

Uchaguzi huo ulikumbwa pia na machafuko ya kabla ya uchaguzi na kupelekea mauaji ya watu takribani 30 huku kukiwa kuna hofu kwamba machafuko na migogoro huenda yakajirudia kama ilivyotokea mwaka 2010 na 2011 ambayo yalisababisha mauaji ya takribani watu 3000.

Mechi ya Simba na Yanga kuchezeshwa na waamuzi 6
CHADEMA yapata mbunge wa kwanza