Kocha Mkuu wa Manchester United, Erik ten Hag amefichua kwamba Alejandro Garnacho aliondolewa baada ya mechi mbili za kwanza za msimu huu kwa sababu uchezaji wake haukuridhisha.
Garnacho alianza dhidi ya Wolves na Tottenham Hotspur Agosti, lakini aliachwa nje ya timu kwa mechi tano kabla ya kurejea na bao katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Crystal Palace juzi Jumanne (Septamba 26).
Lilikuwa bao la kwanza kwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 19 msimu huu na Ten Hag amemtaka Mshambuliaji huyo kuendelea kuimarika.
“Umeona mwanzoni mwa msimu tulimchezesha, mchango wake haukuwa mzuri,” alisema Ten Hag.
“Unaona siku zote ni tishio kwenye mchezo hata asipocheza vizuri, anatakiwa kujifunza anapofanya kazi yake, atakuwa na wakati wake na atakuwa na maamuzi kwa sababu ana sifa kubwa.
“Nadhani ni kawaida kabisa kwa mchezaji wa umri wake kuwa kuna nafasi ya kuimarika sana, kila mtu anampenda, mashabiki wanampenda, timu inampenda, mimi nampenda, lakini pia lazima tudai kutoka kwake.”
Pamoja na Garnacho, Ten Hag pia aliwaanzisha Mason Mount, Raphael Varane na Harry Maguire huku United ikijikatia tiketi katika raundi ya nne ya Kombe la Carabao.