Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Olympic Lyon Alexandre Lacazette ameendelea kusisitiza suala la kutaka kuondoka katika kipindi hiki cha dirisha la usajili.

Lacazette mwenye umri wa miaka 25, amekua akihusishwa na mpango wa kutaka kusajiliwa na washika bunduki wa kaskaini mwa jijini London (Arsenal), lakini dili lake limekua likikwamishwa na suala la ada yake ya usajili.

Arsenal waliwahi kuwasilisha ofa ya Euro milion 35, kwa ajili ya usajili wa Lacazette, lakini uongozi wa Lyon uligoma kumuachia kwa madai ya kiasi hicho hakiendani na thamani ya mshambuliaji huyo.

Lacazette aliendelea kuweka wazi msimamo wake wa kutaka kuondoka mjini Liyon, mara baada ya mchezo wa ufunguzi wa ligi ya nchini Ufaransa (Ligue 1) uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita (jana), ambapo alishuhudiwa akipachika mabao matatu pekee yake dhidi ya Nancy.

Alisema yupo tayari kuondoka na hatokua na suala la kusita endapo klabu yoyote itawasilisha ofa itakayoonekana inafaa mbele ya viongozi wa Lyon.

“Nipo tayari kucheza popote pale, lakini itategemea na uongozi wa Lyon kama utavutiwa na ofa itakayotumwa katika kipindi hiki, Lakini nipo sawa na ninafurahia mazingira ya hapa, japo ni hamu ya kutaka kucheza soka mahala pengine.

“Nafahamu kuna ofa kadhaa zimeshawasilishwa kwa ajili yangu, na zimekataliwa, lakini jambo hilo kwangu haliniumizi kwa sababu kinachofanyika ni kutazama thamani niliyo nayo kwa sasa. Nimefanikiwa kufunga mabao matatu katika mchezo huu, najua kwa wale wanaohitaji huduma yangu katika kipindi hiki watavutiwa zaidi na ndio maana nimesisitiza sina haraka na ninafurahia mazingira ya hapa.” Alisema Lacazette alipohojiwa na Canal Football Club.

Nay wa Mitego kafunguliwa, 'Pale Kati' bado kifungoni
Wekundu Wa Msimbazi Kuingia Darasani