Mshambuliaji kutoka nchini Ufaransa Alexandre Lacazette amesema kuna haja ya wachezaji wa Arsenal kukitumia kipindi cha mapumziko ya kupisha michezo ya kimataifa (timu za taifa), ili kutuliza akili na kujipanga upya kabla ya kuendelea kwa mshike mshike wa ligi kuu ya soka nchini England na michuano mingine.
Lacazette ametoa kauli hiyo kufuatia kikosi cha Arsenal kuwa na mwenendo mbaya kwa siku za karibuni, huku kikikubali kupoteza dhidi ya Leicester City mwishoni mwa juma lililopita, kwa kufungwa mabao mawili kwa sifuri.
Mshambuliaji huyo amesema ni wazi wachezaji wenzake wa klabu hiyo ya jijini London wameonyesha kuchoka na kukata tamaa na hali ya matokeo iliyowakabili kabla ya mchezo wa Jumamosi, hivyo anaamini wakati wa mapumziko watajitahidi kurejesha hali zao vyema na kurejea katika mapambano wakiwa kamili.
“Tumekosa hali ya kujiamini, tunahitaji kukitumia kipindi cha michezo ya kimataifa kutuliza akili zetu na kujipanga upya,” alisema Lacazette.
“Nina matumaini kila kitu kitakua vizuri pindi tutakaporejea katika harakati za kusaka alama tatu katika ligi na michuano mingine tunayoshiriki. Tunatakiwa kuwa na mtazamo chanya kila tutakapoingia katika mapambano.”
“Tulisikitishwa sana na matokeo ya Jumamosi, tulipoteza nafasi nyingi kipindi cha kwanza, na wapinzani wetu (Leicester City) walitumia udhaifu wetu kutushinda kipindi cha pili.”
“Tunapaswa kurejea katika hali yetu ya kushindana kama ilivyokua zamani. Ninaamini kila mmoja ana mawazo kama yangu, na hakuna litakalo shindikana.”
Lacazette ameshafunga mabao mawili tangu kuanza kwa msimu huu, na hajaitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Ufaransa ambacho kitakabiliwa na michezo ya kuwania kufuzu fainali za Ulaya (Euro 2020) dhidi ya Moldova na Albania.
Baada ya michezo ya kimataifa, Arsenal itacheza nyumbani (Emirates Stadium) dhidi ya Southampton, kisha itazikabili Norwich, Brighton na West Ham.