Klabu ya Liverpool ina matumaini ya kumng’oa Brighton Kiungo kutoka Argentina Alexis Mac Allister wakati wa usajili wa majira ya kiangazi (Mwishoni mwa msimu huu) kwa kumtamanisha na dau mara tatu la mshahara wake wa sasa wa kila juma, endapo atakubali kutua Anfield.
Liverpool inajiandaa kufanya mabadiliko makubwa kwenye safu yao ya kiungo dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi, kukiwa na orodha ndefu ya wachezaji wanaotarajia kuonyeshwa mlango wa kutokea huko Anfield.
Alex Oxlade-Chamberlain, Naby Keita na James Milner Wote wanatarajia kuondoka wakati mikataba yao itakapofika tamati mwishoni mwa msimu huu.
Kuondoka kwao kutaacha mapengo kwenye kiungo, hivyo Liverpool itahitaji kuleta viungo wapya kuja kuziba nafasi hizo.
Muargentina, Mac Allister amekuwa kwenye kiwango bora sana huko Brighton na hilo limemvutia kocha wa Liverpool, Jurgen Klopp, anamtaka wakafanye kazi pamoja huko Anfield.
Na katika kulainisha uhamisho huo, Liverpool imemwambia Mac Allister watampa mara tatu ya mshahara wake anaolipwa kwa sasa huko Amex kama tu atakubali kutua Anfield.
Jambo hilo litamfanya Mac Allister awe na uhakika wa kulipwa zaidi ya Pauni 150,000 kwa wiki kama atakubaliana na ofa hiyo ya Liverpool, ambayo pia itafanya kuwa kwenye timu yenye uwezo wa kushindania mataji.
Huko Brighton, Mac Allister amebakiza miaka miwili kwenye mkataba wake wa sasa, lakini ndani yake kuna kipengele cha kuongeza mwaka zaidi. Msimu huu, Mac Allister amefunga mabao 10 na kuasisti mara mbili katika mechi 35 alizocheza.