Klabu ya Arsenal, huenda ikakubali kumuachia mshambuliaji wake kutoka nchini Chile Alexis Sanchez mwishoni mwa msimu huu, kufuatia sintofahamu inayoendelea kuchukua nafasi katika suala la kutosaini mkataba mpya.
Arsenal wapo tayari kumuuza Sanchez kwa mabingwa wa soka nchini Ufaransa Paris Saint-Germain, ambao wameonyesha nia ya dhati ya kumsajili.
Dhumuni la The Gunners kufikiria biashara hiyo, limetokana na hitaji la kutaka kumpeleka mbali na mji wa London mshambuliaji huyo, ambaye ananyatiwa na The Blues (Chelsea).
Taarifa za awali zinaeleza kuwa PSG wapo tayari kutuma ofa ya Pauni milioni 50 huko kaskazini mwa jijini London, ili kufanikisha usajili wa Sanchez wakati wa usajili wa majira ya kiangazi.
Hata hivyo bado meneja wa Arsenal Arsene Wenger, ana matarajio makubwa ya kuendelea kuzungumza na mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ili akubali kusaini mkataba mpya.
Kuhusu suala la ahadi ya kumlipa mshahara wa Pauni laki tatu (300,000) kwa juma, Wenger amekanusha taarifa hizo ambazo zilisambaa katika mitandao ya kijamii mwishoni mwa juma lililopita.
Wenger aliwaambia waandishi wa habari, hajawahi kumwambia ama kumuahidi mshambuliaji huyo mshahara wa Pauni 300,000 kwa juma, zaidi ya uzushi huo kupita katika mitandao ya kijamii.
Sanchez tayari ameshaifungia Arsenal mabao 22 msimu huu, na amekua msaada mkubwa katika kikosi cha The Gunners, tangu aliposajiliwa Emirates Stadium mwaka 2014, akitokea FC Barcelona.