Washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London watamuweka sokoni mshambuliaji wao kutoka nchini Chile Alexis Sanchez kwa dau la Pauni milioni 50, endapo ataendelea kushikilia msimamo wa kugoma kusaini mkataba mpya.
Arsenal imesitisha mazungumzo ya kumnsainisha mkataba mpya mshambuliaji huyo, sambamba na kiungo kutoka nchini Ujerumani Mesut Ozil hadi mwishoni mwa msimu huu, na kama mambo yataendelea kuwauwia vigumu watampiga bei kwenye klabu yoyote itakayokua tayari kulipa kiasi hicho cha pesa.
Wakala wa Sanchez anatajwa kuongoza msimamo wa mshambuliaji huyo wa kukataa kusaini mkataba mpya kwa shinikizo la kutaka alipwe mara mbili ya mshahara anaoupokea kwa sasa Pauni 130,000, ili alingane na wachezaji wengine kama Zlatan Ibrahimovic, Paul Pogba na Sergio Aguero.
Sanchez na Ozil wamesaliwa na miezi 15 kwenye mikataba yao ya sasa, hali ambayo inaendelea kuhatarisha mpango wa klabu ya Arsenal wa kuendelea kuwamiliki kwa msimu mmoja ujao.
Klabu ya Atletico Madrid imeshaonesha nia ya kutaka kumsajili Sanchez mwishoni mwa msimu huu, ili kuziba pengo ambalo huenda likaachwa na mshambuliaji wao kutoka Ufaransa Antoine Griezmann, ambaye thamani yake ya Pauni milioni 80 imeshatangazwa kwa klabu zinazomuwania.
Klabu nyingine zinazompigia hesabu Sanchez endapo atawekwa sokoni na The Gunners wakati wa usajili wa majira ya kiangazi ni FC Bayern Munich, Chelsea, Manchester City, Manchester United na Juventus.