Tuzo maarufu ziitwazo African Entertainment Awards USA (AEAUSA) 2021 hatimaye zimerejea tena zikiwa zimesheheni majina kadhaa ya vijana kutoka Tanzania wenye kuwakilisha Tasnia tofauti tofauti nchini.
Kupitia mtandao maalumu wa tuzo hizo yamewekwa majina ya walioteuliwa kuwania tuzo hizo kwa msimu huu wa mwaka 2021, ambapo majina kadhaa yamefanikiwa kupita akiwamo msaanii kinda kwenye muziki wa Bongo fleva nchini Mac Voice ambaye kwa mara ya kwanza muda mfupi tu baada ya kutambulishwa rasmi kwenye kiwanda cha muziki amefanikiwa kuingia kwenye orodha ya wanaowania tuzo hizo.
Mac Voice kutoka Next Level Music inayomilikiwa na msanii Rayvanny ana takribani mwezi mmoja tu, tangu kuingia rasmi kwenye kiwanda cha muziki na ametajwa kwenye kipengele cha msanii bora chipukizi kwa mwaka 2021 akichuana na wasanii mbali mbali kutoka nchi za Afrika akiwamo Guch kutoka Nigeria, Jeeba, Avra Star, Oxlade pamoja na Omah Lay.
Wengine kutoka Tanzania walioingia kwenye tuzo hizo ni pamoja na Ali Kiba, Diamond Platnumz, Harmonize, Rosa Ree, Zuchu, Navy Kenzo, Mbosso, Nandy, Rayvanny pamoja na weusi huku watangazaji waliotajwa kuwania tuzo hizo ni Djaro Arungu, Adam Mchomvu pamoja na Lil Ommy.
Katika eneo la mtayarishaji bora wa mwaka Tanzania inawakilishwa na Lizer classic pamoja na Director Kenny kwenye kipengele cha muongozaji bora wa mwaka.
Tuzo za African Entertainment Awards USA zinatarajiwa kutolewa mwaka 2022 huko New York nchini Marekani.