Ni muda wa biashara, bifu tupa kule! Ndivyo unavyoweza kuyakariri maneno ya wataalam wa lugha adhimu ya Kiswahili baada ya Ali Kiba kusema kuwa ameamua kudhamini Wasafi Festival ya WCB.
Mkali huyo wa Seduce Me, leo amejibu maombi ya awali ya Diamond aliyemualika kushiriki katika tamasha hilo na kuimba naye pamoja, akisisitiza kuwa tamasha hilo ni la wasanii wote.
King Kiba ameandika majibu yake kwenye Instagram, akieleza kuwa angependa kushiriki tamasha hilo lakini hataweza kutokana na kuwa na ratiba ya kufanya kazi nje ya nchi, lakini atashiriki kibiashara kwa kuwa mmoja wa wadhamini wa tamasha hilo.
“Pia ndugu zangu #Wasafi tumepata salamu zenu, nashukuru kwa mualiko wenu, ila kwa bahati mbaya sitoweza kushiriki kwa sasa kutokana na majukumu ya kuzindua Mofaya katika nchi zingine. Hata hivyo tusingependa kuwaacha hivi hivi, tupo tayari kuwapa support ya kudhamini tamasha lenu kupitia #MofayaEnergyDrink ili kuweza kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya sanaa yetu Tanzania na Africa . Management #RockstarAfrica yangu tutaendelea kuwasiliana nanyi tuweze kufanya hili jambo kubwa. #MofayaByAlikiba#KingKiba,” ameandika Kiba.
Pendekezo hilo la King Kiba limepokewa kwa mikono miwili na Bosi wa WCB, Diamond ambaye amempa jukumu meneja wake Sallam kuwasiliana na uongozi wa Rock Star Africa ili wakamilishe ushirikiano huo wa kibiashara.
“Limepita hilo Ally K… Sallam (meneja wa WCB) anamcheki Seven Now (Meneja wa Rock Star Afrika),” alijibu Diamond akiweka hashtag za #Mofaya #DiamondKaranga #WasafiFestival