Beki wa Kushoto wa Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly Ali Maâloul amesema wameifuatilia timu ya Young Africans na kubaini ubora na udhaifu wao wanapokuwa katika uwanja wa mapambano.
Kikosi cha Al Ahly kiliwasili jijini Dar es salaam usiku wa kuamkia leo Ijumaa (Desemba Mosi), tayari kwa mchezo wa Mzunguuko wa Pili wa Kundi D, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, utakaopigwa kesho Jumamosi (Desemba 02), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Maâloul ambaye alizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, alisema wamefanya maandalizi mazuri kuelekea mchezo huo, na wanafahamu kila kitu kuhusu wenyeji wao.
Amesema katika mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza ambapo Young Africans ilikubali kupoteza dhidi ya CR Belouzdaad kwa mabao 3-0, walifuatilia kila hatua na kubaini mambo mengi yatakayowasaidia kwenye mchezo wa kesho Jumamosi (Desemba 02).
“Tulifuatilia mchezo wao wa kwanza walipocheza dhidi ya CR Belouzdaad, tunakiri wana wachezaji wazuri na walipambana licha ya kupoteza, baada ya hapo tulifanya maandalizi kwa kutumia udhaifu na ubora wao.”
“Kwa mpango mzuri tuliokuja nao hapa, tunaamini tutapambana ili kufanikisha matokeo mzuri tunayohitaji ili kufanikisha safari yetu ya kwenda Robo Fainali.” alisema Ali Maâloul
Timu hizo zilizopo Kundi D zinakutana katika mchezo huo utakaopigwa majira ya saa l:00 usiku kwa saa za Afrika mashariki, huku Al Ahly ikitoka suluhu katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu ya Misri dhidi ya Smouha na kufikisha pointi 14 nyuma ya vinara Pyramids wenye pointi l6.
Young Africans inahitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kutimiza ndoto zao za kwenda Robo Fainali kupitia kundi hilo kwani baada ya hapo itakwenda nchini Ghana kukiputa dhidi ya Medeama.