Imefahamika kuwa Kamati ya Waamuzi ya Shirikisho la soka nchini TFF itamjadili mwamuzi Ludovic Charles ambaye alichezesha mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya Mbeya City dhidi ya Young Africans, Uwanja wa Sokoine mwishoni mwa juma lililopita.

Kamati ya waamuzi itakutana kujadili mambo kadha ya waamuzi, lakini jina la mwamuzi huyo litakua sehemu ya ajenda, baada kulalamikiwa kufuatia maamuzi alioyachukua kwenye mchezo huo wa mzunguuko wa 19 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mwamuzi Ludovic alipata wakati mgumu kwa changamoto ya kulalamikiwa na wachezaji wa timu zote mbili kwa nyakati tofauti za mchezo huo, hali ambayo iliongeza ‘Pressure’ kwa mwamuzi huyo.

Hata hivyo mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi Tanzania, Sud Abdi Mohammed amesema kuwa hawezi kuzungumzia maamuzi ya kwenye mchezo huo wa Mbeya City na Young Africans kwa kuwa ipo kamati inayoshughulikia makosa.

“Ukitaka nizungumzie maamuzi ya mchezo wa Mbeya City na Young Africans huo kwa sasa sitaweza kuzungumzia kwa kuwa  ipo kamati maalumu ambayo huwa inakaa kujadili masuala yanayohusu maamuzi.

“Ikiwa nitasema nizungumzie jambo hilo ninaweza kuonekana ninamtetea ama kumkandamiza hivyo hilo tuachie kamati itafanya kazi yake.”

“Ila kabla ya mzunguko wa pili kuanza tulitoa mafunzo ya vitendo na nadharia kwa muda wa siku tano ambapo tulianza Januari 29 mpaka Februari 2  kwa waamuzi wa Ligi Kuu na tuliwapeleka uwanjani na darasani na tuliwaambia wazingatie sheria na kuchezesha kwa umakini,” amesema Sud Abdi.

Miongoni mwa mambo ambayo yalionekana kulalamikiwa ndani ya Uwanja wa Sokoine ni pamoja na tukio la ‘Fair Play’ dakika ya 25, Mbeya City walikuwa kwenye umiliki wa mpira ila mwamuzi alisimamisha mpira kwa kile alichodai kuwa kuna mchezaji wa Yanga amechezewa faulo.

Dakika ya 67 Deus Kaseke baada ya kuingia akichukua nafasi ya Farid Mussa aliweza kubadili mchezo na Kaseke alionekana kuchezewa faulo ndani ya 18  dakika ya 77 na mchezaji wa Mbeya City.

Tukio hilo mwamuzi alipeta na kuruhusu Mbeya City waendelee na mchezo ndani ya Uwanja wa Sokoine jambo ambalo lililamikiwa na wachezaji.

Bao la Kaseke wa Young Africans, alifunga dakika ya 84 na lilionekana kuwa na utata kwa kuwa mchezaji mmoja wa Mbeya City alionekana akiokoa mpira ule kabla ya kuvuka mstari.

Tukio hilo lilisababisha wachezaji wa Mbeya City kumlalamikia na kipa namba moja Haroun Mandanda alionyeshwa kadi ya njano.

Penati dhidi ya Young Africans iliyotolewa na mwamuzi Lodovic dakika ya 90 baada ya Yassin Mustapha kufuatwa na mpira wakati akiruka ndani ya 18 ililalamikiwa na wachezaji wa klabu hiyo na ilisababisha kadi ya njano kwa nahodha Lamine Moro, huku penati hiyo ikifungwa na Pastory Athanas.

Namungo FC: Figisu za Angola zimetupa somo zito
Makala: Yafahamu Maisha ya Maalim Seif, milima na mabonde