Mshambuliaji wa magojoo wa jiji Liverpool Sadio Mane ametajwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Senegal, ambacho kitacheza michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018 mapema mwezi ujao.

Mane anakabiliwa na majeraha ya nyama za paja aliyoyapata wakati wa michezo ya kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia 2018, iliyofanyika mwanzoni mwa mwezi huu, na hatua ya kuitwa kwake tena kikosini imewashtua wadau wengi wa soka.

Senegal watacheza michezo miwili dhdi ya Afrika kusini Novemba 10 na 14, ambayo itatoa picha halisi kwa taifa hilo kufuzu fainali za 2018 ama la.

Kwa mara ya mwisho Senegal kushiriki fainali za kombe la dunia ilikua mwaka 2002, ambapo walifika hatua ya robo fainali, ili hali kwa Afrika kusini walishiriki mwaka 2010 kama wenyeji.

Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Senegal Aliou Cisse ametetea uamuzi wa kumuita mshambuliaji huyo kikosini, kwa kusema anajua Mane atakua na nafasi ya kuwa sambamba na kikosi chake kutokana na hali yake kuendelea vyema.

“Kwa mtazamo wangu naamini atakua tayari kucheza katika michezo hii miwili ambayo ni muhimu sana kwetu, mpaka kufikia mwezi Novemba atakua ameshapona kwa asilimia 100,” alisema kocha wa Senegal.

“Mpaka sasa ameshafanya mazoezi binafsi ya kukimbia, na itakapofika juma lijalo ataanza kufanya mazoezi magumu kwa ajili ya kujiweka tayari kurejea uwanjani.” aliongeza kiungo huyo wa zamani wa Birmingham City.

Oktoba 10 klabu ya Liverpool ilitoa taarifa rasmi kuhusu mshambuliaji huyo, ambayo iliainisha huenda akarejea tena uwanjani baada ya majuma sita.

Ghana yachanja mbuga FIFA U17, kupambana na Mali
Benchi la ufundi Simba Sports Club lameguka