Seneta wa jimbo la Edo nchini Nigeria, aliyeanzisha kampeni ya kutaka Rais Muhammadu Buhari ajiuzulu au ang’olewe kwa kura ya kutokuwa na imani naye kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma, amedai kupigwa na kijana mdogo.
Seneta Mathew Urhoghide amesema kuwa alifuatwa na kijana mmoja wa kiume ambaye alimzonga na kumpiga kichwani hadharani na kisha kuondoka na kofia yake.
Alisema kuwa kijana huyo alimzonga na kumpiga wiki iliyopita katika uwanja wa ndege wa Benin na kwamba licha ya kuripoti kwa vyombo vya usalama, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya mtu huyo.
“Kama unafanya vitu ambavyo haviendi kwenye muelekeo wa kuwafurahisha, wanakuona kama mtu unayepotoka. Kama ulivyoona wiki iliyopita, kijana mdogo kama yule kunyoosha mkono wake na kumshambulia muwakilishi wa wananchi aliyechaguliwa, tena mwenye cheo cha Seneta, ni aibu kwa nchi hii,” Urhoghide aliiambia Vanguard.
Akizungumzia sababu za kutaka kuendesha kampeni ya kumtaka Buhari kujiuzulu, alisema alifanya hivyo kwa lengo la kulinda maslahi mapana ya umma na kwamba hiyo ni moja kati ya kazi anayopaswa kufanya kama mbunge.
“Sijutii nilichokisema. Nitasimamia nilichokisema. Ni wapi nimemkashifu Rais? Kwa sababu ya ubinafsi wa watu hapa na baadhi wanataka kumuonesha Rais kuwa kila mtu wa Edo ni muoga. Nimekuwa nikisulubiwa katika siku za hivi karibuni kwa nilichokisema bungeni,” aliongeza.
Alidai kuwa hajutii yanayomkuta kwani alijipanga na yuko tayari kuhakikisha kuwa analinda maslahi ya umma na anajua ataadhibiwa na wasiopenda hatua hiyo.
Inadaiwa kuwa Serikali ya Rais Buhari ilitoa kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakikupitishwa na Mamlaka husika kufanya matumizi.