Mfanyabiashara Henry Munisi mkazi wa jiji la Mbeya mwenye umri wa miaka 30 amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kusomewa shtaka la kuchapisha taarifa za uongo zinazomhusisha Rais Dkt, John Magufuli na upotevu wa Sh 1.5 Trilioni.

Munisi anashtakiwa kwa kuandika katika ukurasa wake wa Facebook taarifa za uongo zinazomhusu Rais  Magufuli akizihusisha na ununuzi wa ndege za Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL).

Wakili wa Serikali mwandamizi, Patrick Mwita akitoa madai yake mbele ya Hakimu mkazi mwandamizi, Salum Ally amesema kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo Desemba 28, 2018 akiwa Jijini Mbeya.

Mshtakiwa huyo anadaiwa kuchapisha katika ukurasa wake wa Facebook taarifa inayosomeka “Jinsi Magufuli alivyochota Tril, 1.5 za ATCL akitumia ujanja wake wa kuleta ndege ili atuibie.”

Wakili Mwita ameiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alifanya hivyo huku akijua taarifa hizo ni za uongo na zina lengo la kupotosha umma.

Baada ya kusomewa mashtaka alikana kuhusika na tukio hilo, ambapo wakili wa serikali, Mwita alidai kuwa upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.

Hakimu Ally aliagiza mshatakiwa awe na wadhamini wawili wenye barua za utambulisho watakaosaini bondi ya sh. 500,000, ambapo alifanikiwa kutimiza na kuachiwa kwa dhamana.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 6, mwaka huu.

Urusi yaifyatukia Marekani, yamlinda Rais Maduro
Video: STAMICO kutekeleza maagizo ya viongozi katika sekta ya madini