Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa amesema kwa sasa wanamshikilia Fatuma Selemani Chikawe ambaye ni mkazi wa kigamboni aliyejifanya mtoto wa aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

Mambosasa amesema mwanamke  huyo alikiri mwenyewe  kwa kudai kuwa alisema uongo na amefanya hivyo kwa lengo la kujipatia umaarufu na kumdhalilisha Lowassa.

Hivyo jeshi la polisi linamshikilia kwa upelelezi na mahojiano ambapo ukishakamilika mwanamke huyo atafikishwa mahakamani.

Hata hivyo siku chache zilizopita ilisambaa video ikimuonesha mwanamke huyo akimuomba msamaha Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema, Edward  Lowassa akidai kuwa alifanya hivyo kwa kuwa amekuwa akimtafuta kwa muda mrefu bila mafanikio  hivyo aliamua kutumia njia hiyo ambayo hakutegemea kama ingekuwa hivyo kwani watu wamehusisha tukio hilo na mambo ya kisiasa.

Fatuma Chikawe ni mwanamke aliyejitokeza kupitia zoezi linaloendeshwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda ambaye ameandaa jopo la wanasheria nchini kusaidia kisheria wanawake wa jiji la Dar waliotelekezwa na wanaume waliowazalisha.

Aidha zoezi hilo kwa kiasi kikubwa limezaa matunda ambapo taarifa ya mkuu wa mkoa inasema mpaka sasa zaidi ya wanaume 600 wameitikia wito na tayari wamekubali kulea watoto wao.

 

Khaligraph Jones afunguka mpango wa kufanya kazi na Jay Z
Akamatwa kwa kumtupa mtoto kutoka juu ya paa la nyumba