Mahakama nchini Zambia imemhukumu makamu wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Nevers Mumba kifungo cha miezi mitatu jela kwa makosa ya udanganyifu.

Mumba ambaye alikuwa kiongozi wa chama tawala cha zamani cha- Movement for Multiparty Democracy alihukumiwa kifungo hicho baada ya kukutwa na hatia ya kutoa taarifa za uongo kwa afisa wa jeshi la polisi.

Mwaka 2016, Mumba aliingia bila kibali kwenye ofisi za Shirika la Habari la Zambia (ZNBC) na kulalamikia habari iliyorushwa kuhusu yeye.

Hata hivyo, ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo ulionesha Mumba alimdanganya askari polisi aliyekuwa analinda eneo hilo kuwa alikuwa na makubaliano ya kukutana na mhariri wa kituo hicho.

Mlango aliopitia ulikuwa umezuiliwa kwa watu wasiokuwa na kibali na kwamba watu wote walipaswa kukaguliwa, kinyume cha alichofanya.

Alifunguliwa pia mashtaka ya kuvamia kituo hicho, lakini mahakama iliyatupilia mbali.

Mahakama hiyo imempa nafasi ya kukata rufaa dhidi ya hukumu ya kifungo jela alichopewa.

 

 

Video: Yaliyojiri Mahakama ya Kisutu leo
Picha: Miguna alazwa hospitalini