Rais aliyepinduliwa nchini Mali, Ibrahim Boubacar Keita, amesafirishwa kupelekwa Umoja wa Falme za Kiarabu kwa ajili ya matibabu.
Mwanadiplomasia mmoja ambaye hakutaka kutambulishwa jina lakini anafahamu tukio hilo, amesema hayo na kuongeza kwamba Keita ameondoka akiwa pamoja na mke wake, madaktari wawili, mawakala wanne wa kiusalama na msaidizi.
Jumanne ya wiki hii Keita alipelekwa katika hospitali moja mjini Bamako na kulazwa ambapo hadi siku yaAlhamisi aliporuhusiwa kutoka hospitalini hapo kwa madai kwamba hali yake ya afya ilikuwa inaendelea vizuri.
Tangu Keita mwenye umri wa miaka 75 alipolazwa hospitalini, baada ya kuwekwa kizuizini kwa siku 10 na wanajeshi waliompindua, maswali mengi yameulizwa kuhusu hali yake ya afya.
Katika tukio jingine, mazungumzo kuhusu utakaokuwa utawala wa mpito nchini Mali yameanza jana Jumamosi mjini Bamako na kihudhuriwa na mamia ya wawakilishi wa vyama vya kisiasa pamoja na makundi ya kutetea haki za binadamu .