Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka limewafikisha Mahakamani watuhumiwa wanne ambao wamekutwa na hatia ya makosa ya ubakaji na kuhukumiwa kifungo cha miaka 30 kila mmoja, huku Doreen Lema (30), akifungwa miaka mitano jela kwa kumchoma pasi ya umeme mtoto wake wa kumzaa (7).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo Januari 31, 2023 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP, Justine Masejo amesema waliofikishwa mahakamani ni James Elirehema, John Sanare, Theophili Salaho na Japhet Mungure.
Aidha, katika tukio la pili, Jeshi hilo pia lilimkamata Doreen Lema (30), kwa kosa la kumchoma pasi ya umeme mtoto wake wa kumzaa (7), katika maeneo mbalimbali ya mwili ambapo baada ya kufikishwa Mahakama ya hakimu mkazi wilaya ya Arusha alikutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.
Kamanda Masejo amesema, katika tukio la tatu walifanikiwa kukamata pikipiki iliyokuwa imeibiwa Kijiji cha Qangadend Wilaya ya Karatu ambapo mtuhumiwa Charles Jonas (27) mkazi wa Igunga Mkoani Tabora alikamatwa akiwa usafiri huo wenye namba za usajili SM 12337 aina ya Boxer, mali ya Serikali.
Amesema, mara baada ya uchunguzi wa tukio hilo mtuhumiwa alifikishwa katika Mahakama ya Wilaya Karatu na kusomewa mashtaka ambapo Mahakama ilimkuta na hatia na kumhukumu kifungo cha miaka mitatu jela.
Kufuatia matukio hayo, Kamanda Masejo ametoa wito kwa wananchi kutojihusisha na vitendo vya ukatili wa aina yoyote na kwamba Jeshi la Polisi na kuendelea kutoa taarifa za vitendo hivyo, uhalifu na wahalifu.