Mamlaka za Usalama nchini Kenya, zimeanzisha uchunguzi dhidi ya kifo cha wakili, Paul Gicheru anayetuhumiwa kuwahonga na kuwatisha mashahidi katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), ya kumshtaki Rais William Ruto.
Gicheru, alishutumiwa na waendesha mashitaka wa ICC kwa kuanzisha mpango wa wazi na wenye chuki wa kuwavuruga mashahidi uliofanya kushindwa kuendelea na uchunguzi dhidi ya Ruto, kwa madai ya kuhusika kwake katika ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007-2008 nchini Kenya.
Wakili huyo, ambaye aliyekuwa na umri wa miaka 50, alipatikana amekufa akiwa usingizini Jumatatu usiku nyumbani kwake katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi na katika kujitetea kwake alikanusha mashtaka hayo, mbele ya Mahakama ya ICC, iliyoko The Hague nchini Uholanzi.
Kesi ya Wakili Gicheru, ilianza mwezi Februari mjini hapo The Hague na Waendesha mashtaka wamedai wakili huyo aliwahonga mashahidi hadi shilingi milioni moja za Kenya (takriban euro 8,300) na kuwatishia kwa mtutu wa bunduki.
Ghasia za baada ya uchaguzi kati ya mwishoni mwa 2007 na mapema 2008 zilisababisha zaidi ya watu 1,300 kuuawa na 600,000 kuyahama makazi yao nchini Kenya baada ya uchaguzi wa 2007.
Mwaka 2014, ICC ilifuta kesi dhidi ya Rais wa wakati huo Uhuru Kenyatta kwa tuhuma za uhalifu dhidi ya ubinadamu, aliyedaiwa kuhusika katika ghasia hizo.
Baadaye, Aprili 2016 ilitupilia mbali kesi dhidi ya Makamu wa Rais wa wakati huo, William Ruto na mtangazaji wa Redio Joshua Arap Sang, ambaye naye alishtakiwa katika kesi hiyo hiyo.
Naibu Mwendesha Mashtaka wa ICC, James Stewart alisema mwaka 2016 Gicheru alikuwa ameanzisha mfumo wa kutambua, kupata na kuwashawishi mashahidi katika kesi dhidi ya William Ruto na Joshua Sang.
Kulingana na upande wa mashtaka, mashahidi wanne wakuu, walikanusha ushahidi wao kutokana na hatua alizochukua Gicheru kitu ambacho kilizua maswali na kuanza kwa upelelezi dhidi yake hadi ilipokuja kugundulika kuwa alihonga na kutishia.
William Ruto, alihudumu kwa miaka tisa kama naibu rais wa mkuu wa taifa hilo Uhuru Kenyatta kabla ya kuchaguliwa kuwa rais Agosti , 2022, kwa kumshinda mpinzani wake Raila Odinga.