Mahakama nchini Afrika Kusini imemtia hatiani mwanaume mmoja kwa kosa la kumuua kwa kumchoma kisu mpenzi wake na kisha kuchoma mwili wake ili kuficha.
Sandile Mantsoe mwenye umri wa miaka 28 alikamatwa na jeshi la polisi baada ya mwili wa Korabo Mokoena mwenye umri wa miaka 23, kukutwa karibu na eneo la nyumba yake ukiwa umefukiwa kwenye shimo dogo katika jiji la Johannesburg.
Jaji wa Mahakama hiyo, Peet Johnson alisema kuwa Mantsone amekutwa na hatia ya kumuua kwa kumchoma visu mpenzi wake, na kwamba alikuwa akitunga velelezo vya ushahidi wakati wa utetezi wake.
Mahakama hiyo inasubiri kumhukumu kifungo anachostahili baada ya kumtia hatiani. Kwa mujibu wa sheria za Afrika Kusini, mtu aliyekutwa na hatia ya kuua hukumbwa na kifungo cha maisha kama adhabu ya juu zaidi.
Tukio hilo lilisababisha gumzo kwenye mitandao ya kijamii likilaaniwa vikali huku kukifunguliwa akaunti maalum za kupinga unyanyasaji zilizopewa hashtag ‘MenAreTrash’, yaani wanaume ni takataka.
Mwili wa marehemu ulipatikana baada ya familia yake kutoa taarifa polisi Aprili mwaka jana kuwa ndugu yao amepotea.