Mkuu wa serikali ya Burkina Faso, Ibrahim Traore ambaye alijitangaza kuwa kiongozi mpya wa nchi hiyo kwa kumpindua Luteni Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba, amekutana na Baraza la Mawaziri kufuatia mapinduzi ya kijeshi.
Aliyekuwa kiongozi wa junta Luteni-Kanali Paul-Henri Sandaogo Damiba pia amejitokeza na kusema tayari amejiuzulu kufuatia mazungumzo na kiongozi huyo mpya yaliyofanyika mji mkuu wa nchi hiyo Ouagadougou.
Akiongea na baraza hilo, Traore amesema, “Tunatakiwa kubadili mwendo, tunatakiwa kubadili mwendo, tunatakiwa kwenda haraka, nchi nzima iko katika hali ya hatari, hivyo kila mtu katika ngazi hii lazima awe na kasi na kuachana na mambo yasiyo na lazima.
Amesema, Siwezi kuacha hata sehemu moja ambayo ni muhimu maana hapa Burkina, kila kitu ni cha haraka kuanzia usalama hadi ulinzi, afya, hatua za kijamii, miundombinu, kila kitu ni cha dharura.
Saa chache kabla ya matukio kutokea Ijumaa iliyopita, mamia ya watu walikusanyika katika mji mkuu, Ouagadougou, wakitaka Damiba aondoke, na uwe ni mwisho wa uwepo wa kijeshi wa Ufaransa katika Sahel huku wakiomba ushirikiano wa kijeshi na Urusi.
Hii ni mara ya pili katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja ambapo Burkina Faso imekuwa na mabadiliko ya uongozi wa kimapinduzi na zaidi ya asilimia 40 ya nchi ya Burkina Faso bado iko nje ya udhibiti wa serikali.