Mwanasheria Miguna Miguna ambaye alishiriki tukio la ‘kuapishwa’ kwa kiongozi mkuu wa ngome ya upinzani ya NASA nchini Kenya, Raila Odinga amefunguliwa mashtaka ya uhaini.
Hati ya mashtaka dhidi yake imewasilishwa rasmi katika mahakama ya Kajiado iliyo karibu na jiji la Nairobi.
Katika mashtaka hayo pia, Miguna anashtakiwa kwa kushiriki mkusanyiko usioruhusiwa kisheria na kujihusisha na kitendo cha kihalifu dhidi ya Serikali.
Miguna alikamatwa Ijumaa iliyopita nyumbani kwake na ameendelea kushikiliwa na jeshi la polisi huku haifahamiki mahali au kituo alichopo.
Chama cha Wanasheria nchini humo kimelalamikia hatua ya kutofahamika mahali alipo na kudai kuwa ni kinyume cha haki yake ya msingi.
“Kwa mara nyingine tena, Serikali kwa makusudi inavunja haki ya Miguna kwa kumhamisha bila kumjulisha mwanasheria wake na familia yake kwa lengo la kutaka kuweka ugumu wa kumfikia,” Rais wa chama hicho cha wanasheria, Isaac Okero ameviambia vyombo vya habari.
Leo, vyombo vya habari vimeripoti kuwa Miguna amepandishwa kizimbani katika mahakama ya Kajiado.