Imeelezwa kuwa binti anayedai kuwa alitoa ushahidi wa uongo dhidi ya kijana Tumaini Frank aliyehukumiwa kifungo cha miaka 60 jela mwaka 2018, huenda akakabiliwa na kifungo cha hadi miaka saba jela iwapo itabainika ni kweli alidanganya.
Akifanya mahojiano na Dar24 Media wakili Henry Mwinuka ameeleza kuwa kwa mujibu wa sheria ya kanuni ya adhabu sura ya 16 kifungu cha 102 kinaeleza kuwa kudanganya ni kosa ambalo linaweza kupelekea mtuhumiwa (aliyetoa ushahidi wa uongo) kuhukumiwa kifungo cha hadi miaka saba jela.
“Mahakama inaweza ikaamua kufanya mapitio upya, lakini hawa wenye ushahidi kuupeleka, wazazi wake na ndugu zake (wa kijana) wanatakiwa wawatafute wanasheria waweze kuwasaidia namna ya kufufua hii kesi, kama ushahidi huu utapimwa na kuonekana ni sahihi kwa mizania ya kisheria basi maana yake ni kwamba yule kijana anaweza akaachiliwa huru,” amesema Mwinuka.
Maria Sanga (20), mkazi wa kijiji cha Kilingi Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, amekiri kuwa alimsingizia kijana Tumaini Frank aliyekuwa kidato cha nne kuwa alimpa mimba, ambapo mwaka 2018 Tumaini alihukumiwa kifungo cha miaka 60 jela, na baada ya kukata rufaa hukumu ilipunguzwa hadi miaka 30.
Maria amesema, alipobainika kuwa na ujauzito wazazi wake walimlazimisha sana aseme kuwa Tumaini ndiye aliyempa ujauzito na ikapelekea kijana huyo kuhukumiwa na kukatiza masomo yake.
Tazama mahojiano na mwanasheria hapa chini