Aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Ignas Massawe amefariki dunia.
Kanali Massawe amefariki jana Jumatano Machi 10, 2021 katika hospitali ya Seifee karibu na St. Peters jijini Dar es Salaam.
Kabla ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera mwaka 2011 aliwahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera.
Vilevile, alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Karagwe ambapo alihamishiwa akitokea Kinondoni .
Kanali Fabian Massawe aliwahi kuwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Jitegemee mwaka 1986 hadi 2002.
Fabian Ignas Maswe ni mtoto wa kwanza wa mzee Ignas au Inyasi Mark Massawe na alizaliwa katika kijiji cha Kifuni kata ya Kibosho Magharibi. Elimu ya msingi alisoma Umbwe na Sekondari alisoma Umbwe Sec.
Alijiunga na Jeshi la Wananchi Tanzania mwaka 1979 katika cheo cha Luteni Usu na aliendelea kupandishwa vyeo mpaka cheo cha Kanali alichotunukiwa Januari 2002. Akiwa Jeshini alihudhuria mafunzo lukuki hadi yale ya High Commander Defence Styles.
Kitaaluma, Massawe alikuwa Mwalimu na Mtaalamu wa Maendeleo (Development Studies). Aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Julai 2006, akiwa mtumishi wa umma mwenye uzoefu mkubwa hasa katika elimu ambapo alikuwa Mkuu wa shule maarufu ya Jitegemee ya Jijini Dar es Salaam kwa muda wa miaka 17.
Kwa upande wa michezo, Kanali Massawe alikuwa hazina kubwa ya uendeshaji na usimamizi wa michezo, aidha aliwahi kuwa Mkurugenzi wa Michezo katika Jeshi la Kujenga Taifa, Katibu Mkuu Tanzania Boxing Association, Makamu Mwenyekiti Kamati ya OlImpiki Kanda ya Tano na Mjumbe wa Balaza la Michezo Tanzania.
Watu maaarufu mbalimbali wametuma salamu za rambirambi na kumwelezea vile walivyomfahamu.
Miongoni mwa watu walotuma salamu za rambirambi ni Mtangazaji Mboni Masimba wa kipindi cha “The Mboni Talk Show” ambaye amewahi kuwa mwanafunzi wa Kanali Massawe katika shule ya jitegemee.
“R.I.P Col FABIAN IGNACE MASAWE, nashukuru sana nilipata bahati ya kukufanyia Interview kwenye Thembonishow baada ya zile fujo zote za Utoto tundu wangu wa shule.. Ulitufunza vingi sana wanafunzi wako wa Jitegemee, tulikuwa wakakamavu haswa.. Tutakukumbuka kwa upendo wako, busara zako na discipline uliyoweza kutupa kipindi chote tuko shule? Tangulia Col MASAWE na sisi tuko njiani ?” ameandika Mboni kupitia ukurasa wake wa Instagram akiambatanishana picha aliyopiga na Kanali Masawe enzi za uhai wake.
Hadi anafikwa na umauti, alikuwa Luteni Jenerali wa JWTZ.
Buriani Kanali Fabiana Massawe!