Meneja wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC Massimiliano Allegri, amezungumzia tetesi za kuwa mbioni kuajiriwa na klabu ya Arsenal.
Allegri amelizungumza suala hilo mbele ya waandishi wa habari mara baada ya mchezo wa ligi ya nchini Italia uliochezwa mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Bologna.
Meneja huyo ametajwa kuwa katika mpango wa kupewa ajira Emirates Stadium itakapofika mwishoni mwa msimu huu, ambapo mkataba wa Arsenal na Arsene Wenger utafikia kikomo.
Allegri alisema: “Ninajifunza lugha ya kiingereza, lakini nimekua nikifanya hivi kwa kipindi kirefu.
“Imenishangaza kuona ninahusuishwa na taarifa za kupewa ajira na Arsenal, niliwahi kwenda England sambamba na mwanangu wa kike na nilipokua uwanja wa ndege niliona mtu akisoma gazeti ambalo lilikua na taarifa zinazonihusu, eti inadaiwa nipo katika mpango wa kuajiriwa na Arsenal, ilinishangaza na nilijiuliza linakwenda kutokea leo?”
“Kwa ufupi niwaambie nipo hapa kwa makusudio maalum, na nina furaha ya kufanya kazi na Juventus, na nitahakikisha inakuwa hivyo hadi watakaponitaka kuondoka.”