Kikosi cha Tottenham kitaendelea kupambana bila ya kiungo kutoka nchini England Dele Alli, ambaye bado anasumbuliwa na majeraha ya misuli ya paja.
Alli, mwenye umri wa miaka 22, tayari ameshakosa michezo minne iliyopita, na taarifa kutoka klabuni hapo zinaeleza kuwa, ameanza kufanya mazoezi mepesi ili kuweza kurejea katika hali yake ya kawaida kabla ya kujiunga na wachezaji wenzake kwenye mazoezi ya pamoja.
Kiungo huyo hatokua sehemu ya kikosi kwa leo, ambapo Spurs watacheza mchezo wa mzunguuko watatu wa ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya makundi dhidi ya PSV Eindhoven ya Uholanzi.
Meneja wa Spurs Mauricio Pochettino amezungumza katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo huo, ambapo amesema kukosekana kwa Alli kunaendelea kuwa pigo kwenye kikosi chake, japo ana mipango mbadala ya kuendelea kuziba nafasi yake kama alivyofanya kwenye mchezo iliyopita.
Mbali na Alli, Spurs pia itamkosa beki Danny Rose anaesumbuliwa na majeraha ya nyonga pamoja na Jan Vertonghen (majereha ya misuli ya paja).
Hata hivyo meneja Pochettino amethibitisha atamtumia kiungo mshambuliaji kutoka nchini Denmark Christian Eriksen, baada ya kupata utimamu wa mwili (kuwa FIT).
Spurs na PSV zilipoteza mchezo yote miwili ya kundi B kwa kufungwa na FC Barcelona na Inter Milan, hivyo mpambano wa leo unatarajiwa kuwa na upinzani wa hali ya juu, kutokana na kila upande kuhitaji alama tatu za awali.
Katika ligi ya nchini Uholanzi PSV wanafanya vizuri, kwani mpaka sasa wameshafanikiwa kushinda michezo tisa mfululizo, tofauti na kwa Spurs ambao tayari wameshapoteza michezo miwili kwenye ligi kuu ya England.